Monday, April 23, 2007

Nimerudi tena Jamani. Baada ya kufuta vumbi nyumbani na kusalimia mtaani nikaona ngoja niwabeep (au niwa dipu kama anavyosema Chesi Mpilipili) wale walionitembelea wakati sipo na kuacha ujumbe na wale waliopita kimyakimya. Katika mihangaiko yangu nilifika pale Parisi, Ufaransa na nilitembelea ule mnara wao maharufu (ingawa walitaka kuuondoa mwanzoni) wa Eiffel. Kilichonifurahisha pale Kileleni niliona wameonyesha ni umbali gani uliopo kutoka Hapo Kileleni hadi Mwanza na Dar es salaam.
Angalia pale juu kileleni ndio kuna hayo maandishi hapa chini



Huu ni umbali Kutoka Kileleni mwa mnara wa Eiffel Kuelekea Mwanza.



Na huu ni umbali Kuelekea Dar es salaam.





Thursday, April 12, 2007

BLOGU ULIYOTEMBELEA KWA SASA MWANDISHI WAKE HAYUPO TAFADHARI TEMBELEA TENA BAADAE.
(Nina mizunguko miwili mitatu inayoninyima nafasi ya kuandika nikimaliza nitarudi tena)

Friday, March 30, 2007

IMANI ZETU INAKUWAJE?

Siku moja (Miaka kadhaa iliyopita baada ya septemba 11 ya marekani) nikiwa katika daladala, si unajua kwenye dala dala (hasa vipanya,ila niliyokuwa mimi ilikuwa ngarangara) mtu anaweza akaanzisha hoja/swala/hadithi/mchapo/swali ambalo abiria wote ndani ya daladala wanaanza kuchangia kila mtu kwa mtazamo wake... basi nikiwa ndani ya hilo dala dala ilikuwa usiku umeingia na jamaa wengi ndani ya dala dala walikuwa wanaonekana kuchoka kutokana na mihangaiko ya siku basi walikuwa kimya ila kulikwa na bwana mmoja alikuwa nadhani Kasimu wa matumizi (....unaporudi nyumbani unamwambia mama watoto pesa zote umeibiwa....NADHANI UNANIELEWA HAPA KWA WASIOELEWA ALIKUWA AMELEWA POMBE) basi jamaa yule kweli zilikuwa zimemkamata (ila sikuwa na uhakika ni za aina gani alikuwa amekunywa maana mimi nilikuwa mbali nae kidogo hivyo ile harufu haikunifikia ) kama kawaida ya makonda nao huwa hawachelewi kwa kejeli zao, basi konda aliendelea na kejeli kwa bwana Kasimu wa matumizi, yule jamaa baada ya kuona ni yeye tu na konda wanaobishana na yeye kuelekea kushindwa aliamua kutugeukia abiria,.... basi akaanza hivi...!
Kasimu wa matumizi:Unajua watu wengi wanamuona mmarekani hawapendi waiisalamu, lakini nyie hamjui ....
Konda: Kwanini?Mmarekani bwana hawapendi waisalamu si unaona anavyowafanyia?
Kasimu wa matumizi: aaa mmarekani bwana hana cha muislamu wala mkristo..... nyie si mnasema anawaonea waislamu angalia sasa alivyowafanyia wakristo amewachagulia wakristo askofu SHOGA halafu kawaambia mtake msitake huyu ndiyo askofu, wakristo wote jasho linawatoka...
Nakwambia basi lote tulitokwa na kicheko na mjadala ukaanza.
Basi lengo la hadithi hii ni kuangalia mstakabali huu wa dini zilizoletwa na hawa wageni kwetu, sasa hivi tunaona jinsi dini zilivyo katika migogoro.Ya ukristo.., Kanisa la Kianglikana lina mtafaruku mkubwa hasa umegawanyika kati ya viongozi wa kanisa kutoka Afrika na wale wa Marekani kuhusu swala la ushoga, makanisa yanatishia kukataa misaada toka kwa makanisa ya Kishoga, juzi juzi kanisa la Uswidi nalo limesema litakuwa linabarikia ndoa za mashoga soma hapa (hili ni kanisa la kilutheri )sasa sijui waluteri watanzania wanasemaje?
Ya uislamu kuna wale washia na wale wa sunni ni vurugu tupu..
Kuna rafiki yangu mmoja nae siku moja wakati tukipata moja moto ,moja baridi na moja ya uvuguvugu (kwenye mgahawa wa chuoni tulipokuwa tunasoma) akawa na ubishi na jamaa mmoja alikuja kutuhubiria kuwa hizi mojamoto, moja baridi, na moja ya uvuguvugu hazifai kwa jina la yesu. Basi jamaa akasema mbona kwenye hiyo biblia uliyoshika kuna sehemu imeandikwa kuwa Yesu alitengeneza kinywaji kwenye harusi maana watu mtindi ulikuwa umewaiishia na harusi ikaanza kuwa hakieleweki kitu.. basi jamaa akaanza kutoa maelekezo kuwa oo ile ilikuwa haina kilevi... Kumkatisha jamaa iliaaondoke... (nasi tunendelee na moja yenye umande)basi yule bingwa wangu akamwambia jamaa afadhali waisilamu bwana wao Koran yao imeandikwa Kiarabu na haibadilishwi nyie biblia yenu iko katika kila lugha basi inakuwa mtafaruku maana kila mtu na tafsiri yake...
Kumbuka lakini hawa jamaa wanatoa maoni yao wakati akili yao inaushawishi wa pombe.
Lengo langu mimi nikujiuliza hivi kwanini hawa jamaa walivyokuja kututawala wakasema imani zetu potofu, watu wakakubali bila kujiuliza. Mbona wao hawajafuta imani zao za zamani mpaka leo. Si unajua yale majina ya sayari kwa Kimombo ni majina ya miungu ya Kigiriki? si unajua neno victory linatokana na Mungu wa Kirumi soma hapa . Sina unajua Nike naye alikuwa mungu wa Kigiriki soma hapa.
Basi Lengo langu mimi nikuzungumzia imani zetu za kijadi ambazo nitaendelea nazo Makala ijayo..

Thursday, March 15, 2007

YALIYONIVUTIA MTANDAONI

Leo sina cha kuandika (aa mbona naandika lakini...!) Ninacho cha kuandika, katika pilikapilika zangu za kufanya mkono uende kinywani nimesahau kile kijiti changu (memory stick) cha kuhifadhi kumbukumbu ambacho mara nyingi huwa nakitumia kuhifadhi maandishi yangu mengi, na jamaa mmoja ambaye amenifahamisha anacho, muda wa kuonana nae kwa leo hana basi lengo nililokuwa nataka kufanya leo limeshindikana nikasema lakini nina muda wa kuaandika mawili matatu hapa, basi leo ninaandika yaliyonivutia katika pitapita zangu mtandaoni.
Ngoja nianze na "Blooks prize" vitabu 15, kutoka nchi tano tofauti vimetajawa ambavyo vitashiriki katika kuchaguliwa kupata zawadi ya lulu. Blooks ni vitabu ambavyo vinatokana na blogu, yaani yale mambo yako uliyoyaandika unayafanya kitabu. Mshindi wa mwaka jana alikuwa aliyekuwa na blogu amabayo aliandika MWAKA WANGU WA KUPIKA VIBAYA/HATARI (MY YEAR OF COOKING DANGEROUSLY) na inasemekana ameuza kopi 100,000 na inategemewa sinema kutengenezwa.
Wakenya nao wamenifurahisha na hii tovuti yao ya mzalendo waone hapa Hii ilianza baada ya wabunge wakenya kujipandishia mishahara mwaka 2003..lakini watu walikuwa hawajui nini hasa wafanyacho basi wakaanzisha mzalendo ambapo wanaandika kuhusu kila mswaada upitao bungeni, kila hotuba na kila mbunge aliye katika bunge wasome hapa

Lingine ni lile sakata la bomba la mafuta kwenda kanda ya ziwa ambapo mkataba wa dollar 2.6 billion umepatiwa Kampuni za Kigeni unaolalamikiwa na wazawa wanaosema wamenyanganywa tenda limechukua sura mpya baada ya Kuonekana kuwa Chama cha Mapinduzi kina mkono wake hapo kupitia kampuni ya chama iitwayo Tanzania Green company Limited soma zaidi kuhusu sakata hilo hapa.
Heee......Alamsiki.. (jamaa mwenye kijiti changu anasema kapata muda mchache wa kuonana na mimi ngoja nimuwahi..!)

Tuesday, February 27, 2007

MASIMULIZI YA SINEMA-THE CONSTANT GARDENER

Unakumbuka enzi zile (wale tulioiishi enzi hizo,ingawa sasa nasikia katabia haka kameanza tena)za kwenda kwenye majumba ya sinema kuangalia sinema mbalimbali? Nakumbuka majumba ya sinema yalikuwepo mikoa mingi Tanzania inagawa dari salama yalikuwa mengi akina Drive in, (hapa kama ulikuwa hunakitu unaangalia sinema bubu...nitarudi kwenye hili),New chox,empire,Avalon. Kule mwanza nasikia kulikuwa na majumba mawili ya sinema nakumbuka moja tu Liberty, mji Kasoro Bahari nayo kulikuwa mawili nakumbuka Sapna, huko mbeya au Iringa nako kulikuwa na....mmh nimesahau. Basi enzi hizo nakumbuka kulikuwa na mabingwa wa kusimulia zile sinema hata kama mliiona wote basi mtaanza kusimuliana tena...tena na tena hata kama wengi wetu wakati huo hata kimombo hatujui basi utasema kila kitu jamaa walivyokuwa wanasema kwenye hiyo sinema...au wakati wa sinema yenyewe watu watapiga makelele..angalia nyuma wewe!!!jamaa anakuja kukuua! au kama pale Drive in kwa nje, jamaa anakusimulia kama anasikia vile. Ilikuwa raha mstarehe bwana enzi hizo nakwambia kama ni shule basi wanafunzi wote wanaweza kuja kama kuna sinema maarufu mjini na wakakusimulia mwanzo hadi mwisho lakini hawajaiona wao ila wamesimuliwa lakini wanakusimulia bila kukosea (ndio na kuongezea chumvi...he! he! he!)
Lengo langu basi mimi leo ni Kukusimulia moja ya sinema ambayo inanifikirisha sana mpaka leo hii sinema sasa nimeisha iangalia mara tatu. Sinema hii inakufanya ufikiri zaidi kwa mambo mengi yanayotokea katika nchi zetu (wao wanaziita zinazoendelea).
Sinema hii inaitwa The constant Gardener.
Sinema hii inaanza kwa kuonyesha watu wawili walioingia katika mapenzi ya ghafla baada ya kuoana wanafunga safari kwenda kuishi afrika(kenya) Kwa sababu Bwana na mfanyakazi wa serikali ya Uingereza,baadae Bibi anauwawa pamoja na Dereva wake mwafrika(inapakazwa kuwa mumewe ndio kamfanyizia kwa sababu ana husiano wa kimapenzi na huyo mwafrika) ..basi Bwana ndio anafanya kazi ya kupeleleza kwanini kipenzi chake kimeuwawa anakuja kugundua kuwa mkewe alikuwa akichunguza uharamia ambao makampuni ya madawa yalivyokuwa yakifanya kwa kutumia wananchi bila ya wao kujua kama mahabara zao ,yaani kujaribia madawa yao.
Hii sinema inaelezea makampuni ya madawa ambyo yanajaribu madawa yao kwenye nchi zetu masikini kwa sababu watu hawa hawana faida yoyote kwao na kwasababu viongozi wao pia hawawajali raia wao.
Ni kweli magonjwa yamekuwa mengi na watu wanaitaji dawa lakini utaratibu wa kupata dawa inayotibu ni mrefu na wa gharama kubwa hivyo makampuni yanatafuta njia nyingi za kupunguza gharama na urefu huu kwa kututumia sisi tusio na uwezo na waangalizi wetu wanatuuza. Mara ngapi umesikia dawa za Malaria zimeingia Tanzania baada ya muda unaambiwa hazifai, zinaletwa dawa za kila aina kwa kila magonjwa baada ya watu kupona wanadhurika halafu zinaondolewa jiulize inakuwaje hapa? Kuna mchezo mchafu sana tuanachezewa hapa inabidi kuwa makini sana ....kama hujaiona hii sinema naomba uitafute uiiangalie kama umeiiona iiangalie tena !

Tuesday, February 13, 2007

UBEPARI & other kids stuff

Huyu jamaa kanifikirisha sana, anasema kwa kipindi tunachoiishi sasa duniani kuna maendeleo ya tekenolojia kuliko vipindi vyote lakini ikitakiwa kifanyike kitu kimoja cha maana kama kulisha watu walio katika shida inakuwa... mmhh
Anasema jamaa wa magharibi hawana maji kukatika, watoto wanakwenda shule ,kuna kujisika salama lakini je wanajisikia vizuri?
Anasema ubepari ni kama gari bovu ambalo viongozi wanalitengeneza lakini halitengemai wewe unalipia lakini gari lako halitengemai...
Anasema yeye hataki mchango wako bali anataka wewe ujiulize maswali ya hali ya mambo duniani....
Anatoa mfano wa jinsi watoto wakiwa wanacheza huwa wanagombana lakini hupatana baada ya muda mchache lakini hawa watoto ukumbuke hawajajifunza diplomasia yausuluhishi wala nini...inakuwaje huu utaratibu unavyokuja kuharibika na maana yake nini nini?...
Na mambo kadha wa kadha.
Basi msikilize huyu jamaa (anaelezea kwa muda mrefu kidogo hivyo inabidi uwe na muda wa kumsikiliza) ,fuata maelezo yake kwa kumsililiza moja kwa moja kupitia viungo alivyoweka nenda pale anapokuwambia watch online . Huyu jamaa anapatikana hapa. Mimi nakubaliana nae kwa mambo mengi tu aliyoyasema.

Wednesday, February 07, 2007

HADITHI HII KAKUFUNDISHA NANI?

Nadhani ni wengi wanakumbuka msemo huu... umehadithiiaaa weee,.. umemaliza hadithi yako..au..hapana umesiikiliza wee hadithi hadi imekwisha... halafu yule shangazi anakuuliza hadithi hii kakufundisha nani? .... maana yake ni nini? Majibu si mnayakumbuka.
Ngonja ni kupe kisa kimoja kilinitokea wakati huo nikiwa Sekondari. Sekondari ile (sikutajii mpaka unipe mji!...aa wapi huo unanonipa sitaki) naikumbuka kwa sheria zake ,
1.Yaani tulikuwa haturuhusiwi kuchomekea mashati, basi si unajua utukutu wa shule yaani sheria zote unapingana nazo, basi watu walikuwa wanachomekea, ukimuona mwalimu wa nidhamu(alikuwa anaitwa jina la utani Kicheche) au ukiitwa ofisini ndio unachomoa shati(hapo palikuwa patamu hapo hebu jifikirishe mwenyewe!),
2. Shule zote zilikuwa na Lebo/nembo kwenye shati lakini sisi hatukuwa na nembo..na
3...aah ngoja niishie hapo... turudi kwenye kwenye kisa.
Kipindi kile kilikuwa cha mbio za mweng,e basi mwenge ulikuwa unapita pale shuleni. Yule kiongozi wa mwenge kama tujuavyo anakuwa na ujumbe wa mwenge,basi akatoa ule ujumbe wa mwenge(hatasikumbuki ulikuwa nini?) Basi yule jamaa alipomaliza kwa sababu tulikuwa kimya mwanafunzi mmoja aliuwahi ule ukimya akamuuliza yule ndugu AAGH! yule kiongozi wa mwenge. (tena kwa sauti KUUBWAA) HADITHI HIYO KAKUFUNDISHA NANI?.... Basi nakwambia yule kiongozi wa mwenge alibaki mdomo wazi... na shule nzima ilipasuka kicheko. Kilichofuata mwenye unajua...(si adhabu)
Lengo langu la kukuambia kisa hiki ni kukumbusha kuwa kuna maswala mengi ambayo kwa njia moja ama nyingine ni vizuri mtu kuuliza hadithi hii kakufundisha nani?mfano.. Unaposoma kitabu, Gazeti, jarida, unaposikiliza hotuba za watawala,au majibu au utaratibu si vibaya kuuliza haditihi hhi kakufundisha nani au kamfundisha nani au Kuuliza alikwambia maana yake nini? Sio lazima uulize kwa sauti jaribu kujiuliza mwenye ili upate jibu litakalo kufaa. Kuna mambo mengi ambayo tumekuwa tukiyakubali bila kujua maana yake ni nini.
Nitaendelea Kukuletea mifano ya kujiuuliza ..... (ila usiniliuze sasa na wewe hadithi hii kanifundisha nani.teh..tehe..tehe) Baadae.

Tuesday, December 12, 2006

WADAU, WAJASIRI MALI .....LENGO NI NINI?

Mkurabati, semina elekezi, wadau, wajasiriamali nadhani haya maneno (au ni matamshi?) nadhani umeishawahi kuyasikia au kuyasoma. Lakini ebu nukuulize unaweza kuniambia yana maana gani ? kwa kifupi yaani kama unanielezea maana ya kasheshe. Kama unaweza basi yanaelezeka kama huwezi kwanini yanatumika. Sikatai kwamba lugha hukuwa kwa kuingizwa maneno mapya. Lakini langu mimi ni hii tabia ambayo mimi naona ni kiuga kila kitu. Haya maneno kwa uelevu wangu ni matokeo ya tafsiri kutoka kiingereza kwenda kiswahili, hayajazaliwa kama kungàtuka lilivyozaliwa au Kasheshe.Hii ndio mtindo wanakuwa nao wale wanajiita wataalamu wa maendeleo kuja na maneno kama capacity buliding, participatory,beneficiaries ambayo wao kwa wao huwa wanabishana kuhusu maana yake halisi. Juzi juzi nilihudhuria hutuba mmoja ambapo lengo la mtoa hutuba hiyo ilikuwa ni kutambulisha njia mojawapo ya kuleta mabadiliko katika sehemu za kazi ili sehemu ya kazi iwe ni kivutio kwa mfanyakazi ili afanye kazi kwa ubunifu na ufanisi. Lengo hilo lilikuwa gumu kulifikia kwani baadhi ya wajumbe walianza kubishana kuhusu maana ya neno moja `kutafakari`(reflect) basi ikawa huyu anasema hili huyu anasema lile, Yule muhutubu alijaribu kuchangia kidogo ili avute usikivu kwenye mada yake, lakini kuangalia saa... hamadi! muda umekwenda na majadiliano yamefika mbali na lengo lake, basi akasema ukweli wake, kuwa yeye mara nyingi huwa hajali maana halisi ya neno lakini muhimu ni nini kinafanyika au tunakubaliana kuwa hivi ndivyo namaanisha kwa kufanya kwa vitendo.
Haya maneno sasa yanatumika sana kwenye shughuli za kuleta maendeleo.
Kinachonisumbua mimi ni kuwa haya maneno ni matokeo ya kubandika lebo mpya jambo lile ambalo mimi sidhani kama ni jipya. Kwanza kama lengo ni kumendeleza mlala hoi kwanini lugha yake inakuwa ni ngumu kiasi kwamba huyo mlalahoi mwenyewe mlengwa kwake ni vigumu kuelewa. Hebu niambie kama huyu bibi / bwana/mmachinga/mkulima pale kijijini au pale mjini kajinunulia gazeti lake leo kusoma timu yake ya mpira imeshinda jana basi anataka kuweka kumbukumbu, au kuna haditihi/ukurasa wa mapishi anafuatilia na katika hilo gazeti anakutana na kichwa cha Habari WAJASIRIMALI KUPATIWA MIKOPO YA NAFUU. Hebu niambie kweli huyu mwenzetu atakuwa na hamu kweli ya kusoma hiyo habari. Nini kitamvutia zaidi ya neno Mjasirimali kumkimbiza?Kwanini tunatumia maneno haya kama lengo letu ni kufikisha ujumbe kwa watu wote? Ni kitu gani kipya tumekiona kimebadilika tangu huu utaratibu wa kubadilisha maneno umeanza.
Mie mtizamo wangu ni kuwa kama haya maneno yanatumika basi yawe ni marahisi kuhusishwa na maisha halisi ya walengwa na uelevu wao.

Wednesday, November 08, 2006

NGUVU ZA SODA AU.......?

Najuwa wengi tunaufahamu huu msemo wa nguvu za soda.. yaani unaona tumbo limejaa kwa muda baadae ile gesi kutoka unasikia du kumbe hamna kitu tumboni. Basi ndio nadhani wengi ambao mmekuwa mnanitembelea hapa mnaona mbona hamna kipya Ndabuli ameandika au zilikuwa nguvu za soda? La hasha ila nilitingwa na jukumu la ....sijui ni kweli... la kufuta ujinga au kujijaza ujinga..nikaona ngoja ni kaepembeni kidogo, wale walimu waliobobea kwenye vyuo vikuu kuna wakati wanachukua likizo waiita sabbatical(sijui kwa kiswahili) nikaona ngoja na mimi nijipe hiyo lakini wapi nikaona nina kitu...wanasema ni ka ugonjwa ... yaani ni teja la kompyuta! Kila nikikaa karibu yake nikisema niandike mambo mengine basi vidole vinaniwashwasha inabidi kuanza kuangalia blogu mbalimbali,lakini si yangu, (si ni ya kwangu najua nini kilichomo)...aah lakini kumbe watu wanaacha maoni.
Basi nikakuta Bwana Kitururu kaacha swali. Bwana Kitururu swali lako nalijibu kuwa kaa mkao wa kula ile Habari nitaimalizia. Kama wahenga walivyosema ahadi ni deni basi hilo deni nitalilipa. Nikakutana tena na Bwana Ngurumo ananipa heko zake na kunipiga na swali. Bwana Ngurumo nimependa swali lako na majibu yangu ni kuwa nimependa kujipa jina moja kwani ni rahisi kwa watu kulikumbuka hilo jina na jina hilo halitoi picha au mtazamo wa muelekeo wowote ambao utamfanya mtu kutotaka kusoma (au kusoma ..mmh sijui?) blogu yangu. Jina hili pia lina historia yake ambayo inahusiana na kupenda kwangu kuuliza hivi inakuwaje? Napenda pia umoja huu wa jina kwani mtu atatoa maoni yake bila kushawishiwa na jina. Ila mtu akipenda kuwasiliana nami zaidi anaweza kutumia anuani yangu ya barua pepe.Ila Bwana Ngurumo usiwe na shaka sikuziendavyo tutatambulishana.
Basi kwa kumalizia nitajitahidi sasa kuandika mambo yanayonikuna na mambo haya ni mengi,sitabobea katika swala moja tu, ni lolote litakalo nikuna ..mbona yapo mengi, elimu, siasa, historia,vichekesho..na hata habari za kupaka rangi ya bluu ya anga(sky blue) kwenye choo kwani rangi hii nasikia inzi hawaipendi (sijui ni kweli?...nalifanyia utafiti) na kadha wa kadha.
Ila nakuomba endelea kunitembelea.

Friday, October 13, 2006

UTAMKIKE KIRAHISI!...NA NANI?

Wiki hii ni wiki ambayo kutakuwa kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ni kumbukumbu ya kufikisha miaka saba tangu alipofariki dunia. Alifariki oktoba 14,1999. Langu mimi si kuzungumzia hizi kumbukumbu...sasa unataka kuzngumzia nini?
Nachotaka kuzungumzia ni kitu kingine kabisa ila kimeanzia kwenye Jina la Nyerere. Ni muda si mrefu ule uwanja wetu tunaoita wa kimataifa wa ndege Dar es salaam, ulibadilishwa jina na kuitwa Mwalimu Julius K. Nyerere International Airport. ...Sasa?..
Lakini sasa nimesikia kuwa eti wameondoa "mwalimu" na "K" ili utajike vizuri,.... ama!!! Utajike vizuri na nani sasa? Hapo kweli nimeshindwa kuelewa kuwa hawa watoa majina wanamtazamo gani? Kwani ni watanzania na wanaoongea kiswahili wangapi wanashindwa kutaja mwalimu! au K! Navyo fikiri mimi hata hilo jina lilivyobadilishwa lilikuwa halijatambuliwa sehemu nyingi ...kivipi?...
Umeisha wahi kujaribu kuangalia au kununua tiketi ya ndege katika mtandao,au kuangalia bei zake,au ratiba kwa safari zianziazo Dar es salaam au Kuishia hapo. Kwa kutumia huo utaratibu mashirika mengi ya ndege na makampuni wakala wa usafiri huwa wakionyesha sehemu uendapo na jina la kiwanja cha ndege lakini mpaka hvi karibuni sijaona ukitambuliwa kama mwalimu K. Nyerere....Sawa.. sasa wewe unachotaka kusema ni nini?
Lakini hili la kubadilisha ili litamkike nimeshindwa kulielewa kama ni kwa ajili ya nani? Kama ni kwa wageni wasiojua Kiswahili, kwanini wasijiufunze kutamaka hilo? sisi ndio tuwabadilishie kwa fadia ipi? Na wao mbona hata kubadilisha kutambua kuwa sio tena Dar es salaam international airport hawajafanya hivyo. Unajua airport moja Thailand inaitwaje? Suvarnabhumi International, Taiwani? unaitwa Taiwan Taoyuan International Airport , na mingine mingi tu inamajina kwa lugha yao. ..Kwa hivyo?... Ni wangapi unaowajua wewe wanaweza kutamka hayo majina? Umeishasikia watu hawataki kutumia uwanja kwasababu hawawezi kuutamka?.....MMMH.
Na kumbuka nimekutana na jamaa wengi wasio watanzania na katika kutambulishana nikisema mimi ni mtanzania utasikia oohh mwalimu nyerere!..... but what does mwalimu mean because I think it is not his really name? Basi inabidi kueeleza. Utasikia.... ooh thats interesting...
Mbona hawajabadilisha The mwalimu nyerere foundation iwe The Nyerere foundation. Hiyo foundation haitakiwi kutamkika? Tena nadhani hiyo ndio watu wantakiwa kuitaja sana maana NADHANI inatoa misaada.
Huu ndio mimi naona ni utumwa wa mawazo. Kwanini tusiendeleze kile tulichonacho? Ndio maana hata Raisi mstaafu wa msumbiji alituaibisha kwa yeye kuongea kiswahili wakati sio lugha rasmi katika nchi yake. Yeye akiwa mstari wa mbele kupigia chapuo lugha hii lakini wenyewe wenye kusema ndio lugha rasmi tuko kimya.Hili jambo linanifikirisha sana je ni utumwa wa akili au ni kutokujua?

Sunday, October 08, 2006

WARUSI MHH..NINA WASIWASI!

Jumamosi ya tarehe 7 oktoba 2006 nimesoma na kusikia kuwa mwandishi mmoja wa habari wa urusi Anna Politkovskaya ameuwawa kwa kupigwa risasi bonyeza hapa kusoma inasemekana mwandishi huyu wa habari alikuwa mstari wa mbele katika kuandika habari za ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Urusi. Na ni wiki hiyohiyo ambapo kulikuwa na mtafaruku kati ya serikali ya Urusi na Georgia uliosababisha Urusi kuwarudisha nyumbani wa georgia kibao kwao bonyeza hapa kusoma. Haya matukio hasa hili la kuwarudisha wageorgia limenifanya nikumbuke unyama ambao warusi wanawafanyia wageni hususan wanaotokea Afrika au weusi (Peter Tosh mwanamuziki wa miondoko ya reggae aliimba mwimbo mmoja unaosema as long as you are blackman you are an African,no matter where you are coming from,Bonyeza hapa usome beti za wimbo huo. Haijali unatokea wapi,iwapo wewe ni mweusi ni mwafrika) Huko Urusi hasa mji wa st.petersburgh watu weusi wamekuwa wakiuwawa kwa wingi na bila ya watu kupiga makelele kama yanayopigwa sasa bonya hapa kusoma. Sipingi watu kupiga Kelele ila naona kelele zenyewe zinapigwa kwa kuangalia rangi. Najua kuwa sehemu nyingi duniani hali ndivyo hivyo ilivyo lakini, Juzijuzi raisi Urusi alifanya safari ya Afrika (kuna mwanablogu mmoja au Habri mmoja sikumbuki nilisoma wapi waliipa jina habari hiyo the scramble for Africa) na hakuna sehemu niliyosikia kuwa hili jambo likizungumzwa. Ndio maana nasema Urusi... mmhh. Hasa kwa wale wanaopata scholarship za Kwenda huko.

Tuesday, October 03, 2006

WANASEMA KWELI

Katika pitapita yangu kama kawaida katika blogu mbalimbali nimekutana na hii ya Michelle anayeiishi Tanzania. Anaelezea jinsi alivyoshtushwa na kazi aliyopewa ya kuwa mwandishi wa hotuba ya mke wa raisi. Habari yenyewe inapatikana kwa kichwa cha habari New Profession: Speech Writer?? Hebu nipe maoni yako baada ya kusoma hiyo ya habari.

Friday, September 29, 2006

ELIMU GANI?

Katika pita pita kwangu kwenye blogu (huu mjadala wa neno hili kwa kiswahili sijui uliishia wapi) nili kutana na bwana Charahani kichwa cha Habari Tutaosha miguu ya bodi...? bonyenza hapa na Bwana Mjengwa kichwa cha habari Kama si juhudi zako... bonyeza hapa wakizungumzia swala la Elimu basi nikaona nikiweka maoni kwenye blogu zao maoni yangu yatakuwa marefu sana ni bora niyaandike hapa kwangu. Mabwana hawa wamezungumzia vitu vingi ila mimi nachangia kiujumla kuwa swala halisi hapa ni sio ni kwa jinsi gani elimu inachangia kwa maendeleo ya jamii lakini ni Elimu gani inafaa, kwa maendeleo ya aina gani na kwa faida ya nani? Iwapo tutachambua hili ndio tutajua nini kinafanyika kwa sasa hivi na nini chakurekebisha. Unaweza kukuta kuwa linatengenezwa tabaka la watumishi na watumikiwa au vinginevyo kwa jinsi elimu inavyofadhiliwa na kusambazwa kuna uwezekano mkubwa wa kujenga uwiano usio sawa wa kimapato na unajua kinachofuata. Lakini ili kujua hilo lazima tujadili hilo swali letu. Huu utaratibu wa kusema somo hili linafaa na hili halifai nao unatokana na mtazomo wa kusema elimu ni nini? Huu ndio mjadala unaotakiwa.

katika historia watu wamekuwa wakikumbana na ukweli wa mabadiliko yanayowazunguka . Ni rahisi kuona mabadiliko ya muda mfupi yanayoonekana kila siku yanayotuzunguka lakini vigumu kungamua mabadiliko makubwa yanayotokea kwa muda mrefu. kwa mfano wanahistoria wanafikiria kwamba himaya ya Roma ilikufa kwa wakati mmoja katika historia (kila mmoja anatoa sababu yake kuwa ilivyovamiwa na Alaric 410 a.d au kwa kuondoloewa kwa mfalme wa mwisho wa roma 476 ad n.k) lakini kuhusu wenyeji wa Roma waliona vipi haya matukio? Je walijua kuwa baadae hawa wanahistoria watawaeleza kwa ajabu sana kukua na kufa kwa himaya yao? Kwa wao hawakuona kuanguka kwa himaya yao ( kwa karne 3 kati ya miaka ya Marcus Arelius na na kuzidiwa kwa Roma na Barbarians(sijui kiswahili chake ingawa neno hili nalo lina utata wa kihistoria katika lugha hiyo) karne ya 15 A.D. kipindi hiki kilijulikana kama kukua na kufa kwa himaya ya Roma). kwa wao biashara ya himaya yao iliendelea kama kawaida, wafanya biashara waliendelea kuisha kama watawala,matajiri waliendela kuvaa nguo zao za kifahari na maaskari waliendela kupigana na barbarians hata kama ilikuwa ni kwa pesa na sio kwa kulinda Roma. Hivyo hawakufanya kitu ili kulinda himaya yao na ndio kitakachotokea kwetu iwapo hatushtuka. Nitaendelea siku nyingine nimepatwa na mgeni wa ghafla...

Monday, September 25, 2006

TAASISI YA MASOMO YA AFRIKA?

Ni mara nyingi nimeona na kusikia kila chuo kikuu kina Taasisi ya Masomo ya maendeleo,au Taasisi ya Masomo Ya Afrika. Iwe chuo hiko kiko Afrika au Ulaya au Marekani au Asia. Hizi Taasisi zina jishugulisha na kusoma mambo ya Afrika kuanzia Historia,lugha,Uchumi,siasa na kadha wa kadha. Lakini cha kushangaza ni kuwa sijawahi kusikia wala kuona katika vyuo vyetu vikuu vya Tanzania au (Afrika) Hapa nigesisitiza Tanzania, maana kidogo naufahamu zaidi nayo. Kuwa tuna Taasisi ya Masomo ya Ulaya/Marekani/Asia. Hivi ni kweli sisi hatuitaji kuwasoma hawa jamaa au tunasubiri wao ndio watuambie tuwasome nini, mbona wao wanatusoma kwa faida gani? Hebu hawa wasomi wanaosema kwamba katika majadiliano na hawa mabwana kwenye meza tukikaa nao tunakuwa na ufahamu mmoja je ni ya kweli haya? Kwanini sisi hatuna?

Wednesday, September 20, 2006

Daruso Hata Tovuti?

Katika kusoma soma kwa magazeti ya nyumbani katika mtandao ili angalau nijue kinachoendelea nimesoma kuna mgogoro Mkubwa sana kati ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam na Bodi ya mikopo. Jambo moja nililoliona ni ubishi wa gharama za maisha chuoni. Basi katika kutafakari mgogoro huu mawazo yangu yalinipeleka mbali sana. Nikajiuliza hivi Daruso ina tovuti yake? Hilo jambo sijaliona sasa najiuliza hivi hawa wasomi wetu wameshindwa kweli kutengeneza tovuti?Nikajisemea Hawa Daruso hawana tovuti, lakini wana miradi wanaendesha kwani hii miradi inawasaidia katika nini? Nimeona mifano ya vyama vya wanafunzi katika vyuo vikuu nchi nyingine vikiwa na uwezo wa kufungua migahawa yao ambayo inaendeshwa kwa bei za kiuanafunzi. kwanini wanafunzi wasijijenge kiuchumi ilikuondokana na Tatizo kama hili. Nielewavyo mimi hiki chama kipo kisheria na siku moja katika blogu ya bwana michuzi niliona picha moja ikionyesha jinsi eneo la chuo kikuu likiwa linaota majengo ya vitega uchumi, nikajiuliza hawa Daruso nao wananyanyua kitega uchumi chao ili kuondokana na huu mnyanaso nikasema sidhani kama tovuti hawana itakuwa ili wazo. Je, kweli tutaweza kujisadia wenyewe?