Tuesday, February 27, 2007

MASIMULIZI YA SINEMA-THE CONSTANT GARDENER

Unakumbuka enzi zile (wale tulioiishi enzi hizo,ingawa sasa nasikia katabia haka kameanza tena)za kwenda kwenye majumba ya sinema kuangalia sinema mbalimbali? Nakumbuka majumba ya sinema yalikuwepo mikoa mingi Tanzania inagawa dari salama yalikuwa mengi akina Drive in, (hapa kama ulikuwa hunakitu unaangalia sinema bubu...nitarudi kwenye hili),New chox,empire,Avalon. Kule mwanza nasikia kulikuwa na majumba mawili ya sinema nakumbuka moja tu Liberty, mji Kasoro Bahari nayo kulikuwa mawili nakumbuka Sapna, huko mbeya au Iringa nako kulikuwa na....mmh nimesahau. Basi enzi hizo nakumbuka kulikuwa na mabingwa wa kusimulia zile sinema hata kama mliiona wote basi mtaanza kusimuliana tena...tena na tena hata kama wengi wetu wakati huo hata kimombo hatujui basi utasema kila kitu jamaa walivyokuwa wanasema kwenye hiyo sinema...au wakati wa sinema yenyewe watu watapiga makelele..angalia nyuma wewe!!!jamaa anakuja kukuua! au kama pale Drive in kwa nje, jamaa anakusimulia kama anasikia vile. Ilikuwa raha mstarehe bwana enzi hizo nakwambia kama ni shule basi wanafunzi wote wanaweza kuja kama kuna sinema maarufu mjini na wakakusimulia mwanzo hadi mwisho lakini hawajaiona wao ila wamesimuliwa lakini wanakusimulia bila kukosea (ndio na kuongezea chumvi...he! he! he!)
Lengo langu basi mimi leo ni Kukusimulia moja ya sinema ambayo inanifikirisha sana mpaka leo hii sinema sasa nimeisha iangalia mara tatu. Sinema hii inakufanya ufikiri zaidi kwa mambo mengi yanayotokea katika nchi zetu (wao wanaziita zinazoendelea).
Sinema hii inaitwa The constant Gardener.
Sinema hii inaanza kwa kuonyesha watu wawili walioingia katika mapenzi ya ghafla baada ya kuoana wanafunga safari kwenda kuishi afrika(kenya) Kwa sababu Bwana na mfanyakazi wa serikali ya Uingereza,baadae Bibi anauwawa pamoja na Dereva wake mwafrika(inapakazwa kuwa mumewe ndio kamfanyizia kwa sababu ana husiano wa kimapenzi na huyo mwafrika) ..basi Bwana ndio anafanya kazi ya kupeleleza kwanini kipenzi chake kimeuwawa anakuja kugundua kuwa mkewe alikuwa akichunguza uharamia ambao makampuni ya madawa yalivyokuwa yakifanya kwa kutumia wananchi bila ya wao kujua kama mahabara zao ,yaani kujaribia madawa yao.
Hii sinema inaelezea makampuni ya madawa ambyo yanajaribu madawa yao kwenye nchi zetu masikini kwa sababu watu hawa hawana faida yoyote kwao na kwasababu viongozi wao pia hawawajali raia wao.
Ni kweli magonjwa yamekuwa mengi na watu wanaitaji dawa lakini utaratibu wa kupata dawa inayotibu ni mrefu na wa gharama kubwa hivyo makampuni yanatafuta njia nyingi za kupunguza gharama na urefu huu kwa kututumia sisi tusio na uwezo na waangalizi wetu wanatuuza. Mara ngapi umesikia dawa za Malaria zimeingia Tanzania baada ya muda unaambiwa hazifai, zinaletwa dawa za kila aina kwa kila magonjwa baada ya watu kupona wanadhurika halafu zinaondolewa jiulize inakuwaje hapa? Kuna mchezo mchafu sana tuanachezewa hapa inabidi kuwa makini sana ....kama hujaiona hii sinema naomba uitafute uiiangalie kama umeiiona iiangalie tena !