Tuesday, December 12, 2006

WADAU, WAJASIRI MALI .....LENGO NI NINI?

Mkurabati, semina elekezi, wadau, wajasiriamali nadhani haya maneno (au ni matamshi?) nadhani umeishawahi kuyasikia au kuyasoma. Lakini ebu nukuulize unaweza kuniambia yana maana gani ? kwa kifupi yaani kama unanielezea maana ya kasheshe. Kama unaweza basi yanaelezeka kama huwezi kwanini yanatumika. Sikatai kwamba lugha hukuwa kwa kuingizwa maneno mapya. Lakini langu mimi ni hii tabia ambayo mimi naona ni kiuga kila kitu. Haya maneno kwa uelevu wangu ni matokeo ya tafsiri kutoka kiingereza kwenda kiswahili, hayajazaliwa kama kungàtuka lilivyozaliwa au Kasheshe.Hii ndio mtindo wanakuwa nao wale wanajiita wataalamu wa maendeleo kuja na maneno kama capacity buliding, participatory,beneficiaries ambayo wao kwa wao huwa wanabishana kuhusu maana yake halisi. Juzi juzi nilihudhuria hutuba mmoja ambapo lengo la mtoa hutuba hiyo ilikuwa ni kutambulisha njia mojawapo ya kuleta mabadiliko katika sehemu za kazi ili sehemu ya kazi iwe ni kivutio kwa mfanyakazi ili afanye kazi kwa ubunifu na ufanisi. Lengo hilo lilikuwa gumu kulifikia kwani baadhi ya wajumbe walianza kubishana kuhusu maana ya neno moja `kutafakari`(reflect) basi ikawa huyu anasema hili huyu anasema lile, Yule muhutubu alijaribu kuchangia kidogo ili avute usikivu kwenye mada yake, lakini kuangalia saa... hamadi! muda umekwenda na majadiliano yamefika mbali na lengo lake, basi akasema ukweli wake, kuwa yeye mara nyingi huwa hajali maana halisi ya neno lakini muhimu ni nini kinafanyika au tunakubaliana kuwa hivi ndivyo namaanisha kwa kufanya kwa vitendo.
Haya maneno sasa yanatumika sana kwenye shughuli za kuleta maendeleo.
Kinachonisumbua mimi ni kuwa haya maneno ni matokeo ya kubandika lebo mpya jambo lile ambalo mimi sidhani kama ni jipya. Kwanza kama lengo ni kumendeleza mlala hoi kwanini lugha yake inakuwa ni ngumu kiasi kwamba huyo mlalahoi mwenyewe mlengwa kwake ni vigumu kuelewa. Hebu niambie kama huyu bibi / bwana/mmachinga/mkulima pale kijijini au pale mjini kajinunulia gazeti lake leo kusoma timu yake ya mpira imeshinda jana basi anataka kuweka kumbukumbu, au kuna haditihi/ukurasa wa mapishi anafuatilia na katika hilo gazeti anakutana na kichwa cha Habari WAJASIRIMALI KUPATIWA MIKOPO YA NAFUU. Hebu niambie kweli huyu mwenzetu atakuwa na hamu kweli ya kusoma hiyo habari. Nini kitamvutia zaidi ya neno Mjasirimali kumkimbiza?Kwanini tunatumia maneno haya kama lengo letu ni kufikisha ujumbe kwa watu wote? Ni kitu gani kipya tumekiona kimebadilika tangu huu utaratibu wa kubadilisha maneno umeanza.
Mie mtizamo wangu ni kuwa kama haya maneno yanatumika basi yawe ni marahisi kuhusishwa na maisha halisi ya walengwa na uelevu wao.