Tuesday, December 12, 2006

WADAU, WAJASIRI MALI .....LENGO NI NINI?

Mkurabati, semina elekezi, wadau, wajasiriamali nadhani haya maneno (au ni matamshi?) nadhani umeishawahi kuyasikia au kuyasoma. Lakini ebu nukuulize unaweza kuniambia yana maana gani ? kwa kifupi yaani kama unanielezea maana ya kasheshe. Kama unaweza basi yanaelezeka kama huwezi kwanini yanatumika. Sikatai kwamba lugha hukuwa kwa kuingizwa maneno mapya. Lakini langu mimi ni hii tabia ambayo mimi naona ni kiuga kila kitu. Haya maneno kwa uelevu wangu ni matokeo ya tafsiri kutoka kiingereza kwenda kiswahili, hayajazaliwa kama kungàtuka lilivyozaliwa au Kasheshe.Hii ndio mtindo wanakuwa nao wale wanajiita wataalamu wa maendeleo kuja na maneno kama capacity buliding, participatory,beneficiaries ambayo wao kwa wao huwa wanabishana kuhusu maana yake halisi. Juzi juzi nilihudhuria hutuba mmoja ambapo lengo la mtoa hutuba hiyo ilikuwa ni kutambulisha njia mojawapo ya kuleta mabadiliko katika sehemu za kazi ili sehemu ya kazi iwe ni kivutio kwa mfanyakazi ili afanye kazi kwa ubunifu na ufanisi. Lengo hilo lilikuwa gumu kulifikia kwani baadhi ya wajumbe walianza kubishana kuhusu maana ya neno moja `kutafakari`(reflect) basi ikawa huyu anasema hili huyu anasema lile, Yule muhutubu alijaribu kuchangia kidogo ili avute usikivu kwenye mada yake, lakini kuangalia saa... hamadi! muda umekwenda na majadiliano yamefika mbali na lengo lake, basi akasema ukweli wake, kuwa yeye mara nyingi huwa hajali maana halisi ya neno lakini muhimu ni nini kinafanyika au tunakubaliana kuwa hivi ndivyo namaanisha kwa kufanya kwa vitendo.
Haya maneno sasa yanatumika sana kwenye shughuli za kuleta maendeleo.
Kinachonisumbua mimi ni kuwa haya maneno ni matokeo ya kubandika lebo mpya jambo lile ambalo mimi sidhani kama ni jipya. Kwanza kama lengo ni kumendeleza mlala hoi kwanini lugha yake inakuwa ni ngumu kiasi kwamba huyo mlalahoi mwenyewe mlengwa kwake ni vigumu kuelewa. Hebu niambie kama huyu bibi / bwana/mmachinga/mkulima pale kijijini au pale mjini kajinunulia gazeti lake leo kusoma timu yake ya mpira imeshinda jana basi anataka kuweka kumbukumbu, au kuna haditihi/ukurasa wa mapishi anafuatilia na katika hilo gazeti anakutana na kichwa cha Habari WAJASIRIMALI KUPATIWA MIKOPO YA NAFUU. Hebu niambie kweli huyu mwenzetu atakuwa na hamu kweli ya kusoma hiyo habari. Nini kitamvutia zaidi ya neno Mjasirimali kumkimbiza?Kwanini tunatumia maneno haya kama lengo letu ni kufikisha ujumbe kwa watu wote? Ni kitu gani kipya tumekiona kimebadilika tangu huu utaratibu wa kubadilisha maneno umeanza.
Mie mtizamo wangu ni kuwa kama haya maneno yanatumika basi yawe ni marahisi kuhusishwa na maisha halisi ya walengwa na uelevu wao.

Wednesday, November 08, 2006

NGUVU ZA SODA AU.......?

Najuwa wengi tunaufahamu huu msemo wa nguvu za soda.. yaani unaona tumbo limejaa kwa muda baadae ile gesi kutoka unasikia du kumbe hamna kitu tumboni. Basi ndio nadhani wengi ambao mmekuwa mnanitembelea hapa mnaona mbona hamna kipya Ndabuli ameandika au zilikuwa nguvu za soda? La hasha ila nilitingwa na jukumu la ....sijui ni kweli... la kufuta ujinga au kujijaza ujinga..nikaona ngoja ni kaepembeni kidogo, wale walimu waliobobea kwenye vyuo vikuu kuna wakati wanachukua likizo waiita sabbatical(sijui kwa kiswahili) nikaona ngoja na mimi nijipe hiyo lakini wapi nikaona nina kitu...wanasema ni ka ugonjwa ... yaani ni teja la kompyuta! Kila nikikaa karibu yake nikisema niandike mambo mengine basi vidole vinaniwashwasha inabidi kuanza kuangalia blogu mbalimbali,lakini si yangu, (si ni ya kwangu najua nini kilichomo)...aah lakini kumbe watu wanaacha maoni.
Basi nikakuta Bwana Kitururu kaacha swali. Bwana Kitururu swali lako nalijibu kuwa kaa mkao wa kula ile Habari nitaimalizia. Kama wahenga walivyosema ahadi ni deni basi hilo deni nitalilipa. Nikakutana tena na Bwana Ngurumo ananipa heko zake na kunipiga na swali. Bwana Ngurumo nimependa swali lako na majibu yangu ni kuwa nimependa kujipa jina moja kwani ni rahisi kwa watu kulikumbuka hilo jina na jina hilo halitoi picha au mtazamo wa muelekeo wowote ambao utamfanya mtu kutotaka kusoma (au kusoma ..mmh sijui?) blogu yangu. Jina hili pia lina historia yake ambayo inahusiana na kupenda kwangu kuuliza hivi inakuwaje? Napenda pia umoja huu wa jina kwani mtu atatoa maoni yake bila kushawishiwa na jina. Ila mtu akipenda kuwasiliana nami zaidi anaweza kutumia anuani yangu ya barua pepe.Ila Bwana Ngurumo usiwe na shaka sikuziendavyo tutatambulishana.
Basi kwa kumalizia nitajitahidi sasa kuandika mambo yanayonikuna na mambo haya ni mengi,sitabobea katika swala moja tu, ni lolote litakalo nikuna ..mbona yapo mengi, elimu, siasa, historia,vichekesho..na hata habari za kupaka rangi ya bluu ya anga(sky blue) kwenye choo kwani rangi hii nasikia inzi hawaipendi (sijui ni kweli?...nalifanyia utafiti) na kadha wa kadha.
Ila nakuomba endelea kunitembelea.

Friday, October 13, 2006

UTAMKIKE KIRAHISI!...NA NANI?

Wiki hii ni wiki ambayo kutakuwa kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ni kumbukumbu ya kufikisha miaka saba tangu alipofariki dunia. Alifariki oktoba 14,1999. Langu mimi si kuzungumzia hizi kumbukumbu...sasa unataka kuzngumzia nini?
Nachotaka kuzungumzia ni kitu kingine kabisa ila kimeanzia kwenye Jina la Nyerere. Ni muda si mrefu ule uwanja wetu tunaoita wa kimataifa wa ndege Dar es salaam, ulibadilishwa jina na kuitwa Mwalimu Julius K. Nyerere International Airport. ...Sasa?..
Lakini sasa nimesikia kuwa eti wameondoa "mwalimu" na "K" ili utajike vizuri,.... ama!!! Utajike vizuri na nani sasa? Hapo kweli nimeshindwa kuelewa kuwa hawa watoa majina wanamtazamo gani? Kwani ni watanzania na wanaoongea kiswahili wangapi wanashindwa kutaja mwalimu! au K! Navyo fikiri mimi hata hilo jina lilivyobadilishwa lilikuwa halijatambuliwa sehemu nyingi ...kivipi?...
Umeisha wahi kujaribu kuangalia au kununua tiketi ya ndege katika mtandao,au kuangalia bei zake,au ratiba kwa safari zianziazo Dar es salaam au Kuishia hapo. Kwa kutumia huo utaratibu mashirika mengi ya ndege na makampuni wakala wa usafiri huwa wakionyesha sehemu uendapo na jina la kiwanja cha ndege lakini mpaka hvi karibuni sijaona ukitambuliwa kama mwalimu K. Nyerere....Sawa.. sasa wewe unachotaka kusema ni nini?
Lakini hili la kubadilisha ili litamkike nimeshindwa kulielewa kama ni kwa ajili ya nani? Kama ni kwa wageni wasiojua Kiswahili, kwanini wasijiufunze kutamaka hilo? sisi ndio tuwabadilishie kwa fadia ipi? Na wao mbona hata kubadilisha kutambua kuwa sio tena Dar es salaam international airport hawajafanya hivyo. Unajua airport moja Thailand inaitwaje? Suvarnabhumi International, Taiwani? unaitwa Taiwan Taoyuan International Airport , na mingine mingi tu inamajina kwa lugha yao. ..Kwa hivyo?... Ni wangapi unaowajua wewe wanaweza kutamka hayo majina? Umeishasikia watu hawataki kutumia uwanja kwasababu hawawezi kuutamka?.....MMMH.
Na kumbuka nimekutana na jamaa wengi wasio watanzania na katika kutambulishana nikisema mimi ni mtanzania utasikia oohh mwalimu nyerere!..... but what does mwalimu mean because I think it is not his really name? Basi inabidi kueeleza. Utasikia.... ooh thats interesting...
Mbona hawajabadilisha The mwalimu nyerere foundation iwe The Nyerere foundation. Hiyo foundation haitakiwi kutamkika? Tena nadhani hiyo ndio watu wantakiwa kuitaja sana maana NADHANI inatoa misaada.
Huu ndio mimi naona ni utumwa wa mawazo. Kwanini tusiendeleze kile tulichonacho? Ndio maana hata Raisi mstaafu wa msumbiji alituaibisha kwa yeye kuongea kiswahili wakati sio lugha rasmi katika nchi yake. Yeye akiwa mstari wa mbele kupigia chapuo lugha hii lakini wenyewe wenye kusema ndio lugha rasmi tuko kimya.Hili jambo linanifikirisha sana je ni utumwa wa akili au ni kutokujua?

Sunday, October 08, 2006

WARUSI MHH..NINA WASIWASI!

Jumamosi ya tarehe 7 oktoba 2006 nimesoma na kusikia kuwa mwandishi mmoja wa habari wa urusi Anna Politkovskaya ameuwawa kwa kupigwa risasi bonyeza hapa kusoma inasemekana mwandishi huyu wa habari alikuwa mstari wa mbele katika kuandika habari za ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Urusi. Na ni wiki hiyohiyo ambapo kulikuwa na mtafaruku kati ya serikali ya Urusi na Georgia uliosababisha Urusi kuwarudisha nyumbani wa georgia kibao kwao bonyeza hapa kusoma. Haya matukio hasa hili la kuwarudisha wageorgia limenifanya nikumbuke unyama ambao warusi wanawafanyia wageni hususan wanaotokea Afrika au weusi (Peter Tosh mwanamuziki wa miondoko ya reggae aliimba mwimbo mmoja unaosema as long as you are blackman you are an African,no matter where you are coming from,Bonyeza hapa usome beti za wimbo huo. Haijali unatokea wapi,iwapo wewe ni mweusi ni mwafrika) Huko Urusi hasa mji wa st.petersburgh watu weusi wamekuwa wakiuwawa kwa wingi na bila ya watu kupiga makelele kama yanayopigwa sasa bonya hapa kusoma. Sipingi watu kupiga Kelele ila naona kelele zenyewe zinapigwa kwa kuangalia rangi. Najua kuwa sehemu nyingi duniani hali ndivyo hivyo ilivyo lakini, Juzijuzi raisi Urusi alifanya safari ya Afrika (kuna mwanablogu mmoja au Habri mmoja sikumbuki nilisoma wapi waliipa jina habari hiyo the scramble for Africa) na hakuna sehemu niliyosikia kuwa hili jambo likizungumzwa. Ndio maana nasema Urusi... mmhh. Hasa kwa wale wanaopata scholarship za Kwenda huko.

Tuesday, October 03, 2006

WANASEMA KWELI

Katika pitapita yangu kama kawaida katika blogu mbalimbali nimekutana na hii ya Michelle anayeiishi Tanzania. Anaelezea jinsi alivyoshtushwa na kazi aliyopewa ya kuwa mwandishi wa hotuba ya mke wa raisi. Habari yenyewe inapatikana kwa kichwa cha habari New Profession: Speech Writer?? Hebu nipe maoni yako baada ya kusoma hiyo ya habari.

Friday, September 29, 2006

ELIMU GANI?

Katika pita pita kwangu kwenye blogu (huu mjadala wa neno hili kwa kiswahili sijui uliishia wapi) nili kutana na bwana Charahani kichwa cha Habari Tutaosha miguu ya bodi...? bonyenza hapa na Bwana Mjengwa kichwa cha habari Kama si juhudi zako... bonyeza hapa wakizungumzia swala la Elimu basi nikaona nikiweka maoni kwenye blogu zao maoni yangu yatakuwa marefu sana ni bora niyaandike hapa kwangu. Mabwana hawa wamezungumzia vitu vingi ila mimi nachangia kiujumla kuwa swala halisi hapa ni sio ni kwa jinsi gani elimu inachangia kwa maendeleo ya jamii lakini ni Elimu gani inafaa, kwa maendeleo ya aina gani na kwa faida ya nani? Iwapo tutachambua hili ndio tutajua nini kinafanyika kwa sasa hivi na nini chakurekebisha. Unaweza kukuta kuwa linatengenezwa tabaka la watumishi na watumikiwa au vinginevyo kwa jinsi elimu inavyofadhiliwa na kusambazwa kuna uwezekano mkubwa wa kujenga uwiano usio sawa wa kimapato na unajua kinachofuata. Lakini ili kujua hilo lazima tujadili hilo swali letu. Huu utaratibu wa kusema somo hili linafaa na hili halifai nao unatokana na mtazomo wa kusema elimu ni nini? Huu ndio mjadala unaotakiwa.

katika historia watu wamekuwa wakikumbana na ukweli wa mabadiliko yanayowazunguka . Ni rahisi kuona mabadiliko ya muda mfupi yanayoonekana kila siku yanayotuzunguka lakini vigumu kungamua mabadiliko makubwa yanayotokea kwa muda mrefu. kwa mfano wanahistoria wanafikiria kwamba himaya ya Roma ilikufa kwa wakati mmoja katika historia (kila mmoja anatoa sababu yake kuwa ilivyovamiwa na Alaric 410 a.d au kwa kuondoloewa kwa mfalme wa mwisho wa roma 476 ad n.k) lakini kuhusu wenyeji wa Roma waliona vipi haya matukio? Je walijua kuwa baadae hawa wanahistoria watawaeleza kwa ajabu sana kukua na kufa kwa himaya yao? Kwa wao hawakuona kuanguka kwa himaya yao ( kwa karne 3 kati ya miaka ya Marcus Arelius na na kuzidiwa kwa Roma na Barbarians(sijui kiswahili chake ingawa neno hili nalo lina utata wa kihistoria katika lugha hiyo) karne ya 15 A.D. kipindi hiki kilijulikana kama kukua na kufa kwa himaya ya Roma). kwa wao biashara ya himaya yao iliendelea kama kawaida, wafanya biashara waliendelea kuisha kama watawala,matajiri waliendela kuvaa nguo zao za kifahari na maaskari waliendela kupigana na barbarians hata kama ilikuwa ni kwa pesa na sio kwa kulinda Roma. Hivyo hawakufanya kitu ili kulinda himaya yao na ndio kitakachotokea kwetu iwapo hatushtuka. Nitaendelea siku nyingine nimepatwa na mgeni wa ghafla...

Monday, September 25, 2006

TAASISI YA MASOMO YA AFRIKA?

Ni mara nyingi nimeona na kusikia kila chuo kikuu kina Taasisi ya Masomo ya maendeleo,au Taasisi ya Masomo Ya Afrika. Iwe chuo hiko kiko Afrika au Ulaya au Marekani au Asia. Hizi Taasisi zina jishugulisha na kusoma mambo ya Afrika kuanzia Historia,lugha,Uchumi,siasa na kadha wa kadha. Lakini cha kushangaza ni kuwa sijawahi kusikia wala kuona katika vyuo vyetu vikuu vya Tanzania au (Afrika) Hapa nigesisitiza Tanzania, maana kidogo naufahamu zaidi nayo. Kuwa tuna Taasisi ya Masomo ya Ulaya/Marekani/Asia. Hivi ni kweli sisi hatuitaji kuwasoma hawa jamaa au tunasubiri wao ndio watuambie tuwasome nini, mbona wao wanatusoma kwa faida gani? Hebu hawa wasomi wanaosema kwamba katika majadiliano na hawa mabwana kwenye meza tukikaa nao tunakuwa na ufahamu mmoja je ni ya kweli haya? Kwanini sisi hatuna?

Wednesday, September 20, 2006

Daruso Hata Tovuti?

Katika kusoma soma kwa magazeti ya nyumbani katika mtandao ili angalau nijue kinachoendelea nimesoma kuna mgogoro Mkubwa sana kati ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam na Bodi ya mikopo. Jambo moja nililoliona ni ubishi wa gharama za maisha chuoni. Basi katika kutafakari mgogoro huu mawazo yangu yalinipeleka mbali sana. Nikajiuliza hivi Daruso ina tovuti yake? Hilo jambo sijaliona sasa najiuliza hivi hawa wasomi wetu wameshindwa kweli kutengeneza tovuti?Nikajisemea Hawa Daruso hawana tovuti, lakini wana miradi wanaendesha kwani hii miradi inawasaidia katika nini? Nimeona mifano ya vyama vya wanafunzi katika vyuo vikuu nchi nyingine vikiwa na uwezo wa kufungua migahawa yao ambayo inaendeshwa kwa bei za kiuanafunzi. kwanini wanafunzi wasijijenge kiuchumi ilikuondokana na Tatizo kama hili. Nielewavyo mimi hiki chama kipo kisheria na siku moja katika blogu ya bwana michuzi niliona picha moja ikionyesha jinsi eneo la chuo kikuu likiwa linaota majengo ya vitega uchumi, nikajiuliza hawa Daruso nao wananyanyua kitega uchumi chao ili kuondokana na huu mnyanaso nikasema sidhani kama tovuti hawana itakuwa ili wazo. Je, kweli tutaweza kujisadia wenyewe?