Thursday, September 06, 2007

Prof.CHACHAGE, MAMA TERESA

Kama wewe huwa unapita pita hapa kibarazani kwangu utakuwa unashangaa aaah! huyu Ndabuli naye kwa kutofuata ahadi zake ni kiboko ( kivipi?). Si kwenye mtundiko uliopita alisema atazungumzia zaidi kuhusu kisa cha kununua kahawa kwenye bar na Kuhusu kuwashiana taa kwa madereva ..huyu bwana ....#¤%& ....kabisa na hata kwa waliotoa maoni alisistiza hivyo...( kama wewe ndio umenitembelea leo soma makala hiyo ya chini) au bonya hapa.
Ni kweli nimetoa hiyo ahadi na nitaitimiza, ila jambo lingine limenikuna sana nikaona ngonja niliandike hili kwanza...(najua unajiuliza jambo gani tena!)
Wiki hii nimemkumbuka professa Chachage. Nikiwa huku ugenini nilipata kukutana na prof. Chachage akiwa katika mizunguko yake ya kutoa mihadhara mbalimbali. Basi nami nilikuwa mmoja kati ya watu waliohudhuria shughuli ile iliyomleta... siku moja (kati ya siku zile alizokuwa hapa) nilipata/tulipata wasaa wa kukaa naye jioni huku tukipata moja moto moja baridi ..(mmh nimesahau moja baridi nyingine baridi maana huku hakuna za moto..labda chai na kahawa). Katika mazungumzo yetu ya jioni kuhusu mambo mbalimbali ilifika wakati tukiwa tukijadiliana (kulikuwa na wadanganyika wenzangu...oops watanzania wenzangu) likatokea swala moja la kupingana na magazeti yanayoashabikia siasa nizisozipendelea sana.
Huwa na kawaida ya kusubscribe (sijui kiswahili chake jamani..si uniambie kama unajua) magazeti na majarida mbalimbali. Kati ya hayo kulikwa na jarida, sijui gazeti, la Time ambalo hutoka mara moja kila wiki. Baada ya kulisoma kwa muda mrefu niliamua kuachana nalo kwani niliona vingi vinavyoandika humo haviendani na mtazamo wangu, hivyo nikaamua kutolilipia tena...basi prof. Chachage aliposikia hivi aliniambia kitu kimoja sitosahau mpaka leo. Kuwa ni makosa makubwa sana kutosoma mtazamo wa mtu mwenye itikadi ambazo hukubaliani nazo..unakuwa katika mstari mzuri wa kumjua au kujua fikira zake na kuweza kuzipambanisha na zako kwa kumsoma mtazamo wake... nami kweli nilikubaliana naye hiyo niliendelea kusoma lile gazeti la Time(ila niliacha kulilipia.. siku hizi nalisomea makataba).
Gazeti la wiki hii (lenye tarehe ya septemba 3) limekuja na kitu ambacho kinalingana na kitu nilichoandika zama zilizopita kikiwa na kichwa cha habari Imani zetu inakuwaje? Makala yenyewe inaelezea kuhusu Mama Teresa (Unamkumbuka? yule sista wa kikatoliki...enhee yule mshindi wa nishani ya Amani ya Nobel ya mwaka 1979) Msome hapa. Kwamba kwa takribani miaka 50 hakuona uwepo wa mungu.
Katika kitabu kilichotolewa chenye Jina la Mother Teresa: Come Be My light. ambacho kwa wingi kina maelezo ya mawasiliano kati yake na wakubwa zake. Kinaonyesha kuwa kwa karibu nusu muongo wa maisha yake hakuona uwepo wa mungu kwa hali yoyote. Hii ni makala iliyonifikirisha sana. Basi nisimalize uhondo soma mwenyewe makala hiyo hapa. halafu jifikirishe..Baadae!