Wednesday, February 07, 2007

HADITHI HII KAKUFUNDISHA NANI?

Nadhani ni wengi wanakumbuka msemo huu... umehadithiiaaa weee,.. umemaliza hadithi yako..au..hapana umesiikiliza wee hadithi hadi imekwisha... halafu yule shangazi anakuuliza hadithi hii kakufundisha nani? .... maana yake ni nini? Majibu si mnayakumbuka.
Ngonja ni kupe kisa kimoja kilinitokea wakati huo nikiwa Sekondari. Sekondari ile (sikutajii mpaka unipe mji!...aa wapi huo unanonipa sitaki) naikumbuka kwa sheria zake ,
1.Yaani tulikuwa haturuhusiwi kuchomekea mashati, basi si unajua utukutu wa shule yaani sheria zote unapingana nazo, basi watu walikuwa wanachomekea, ukimuona mwalimu wa nidhamu(alikuwa anaitwa jina la utani Kicheche) au ukiitwa ofisini ndio unachomoa shati(hapo palikuwa patamu hapo hebu jifikirishe mwenyewe!),
2. Shule zote zilikuwa na Lebo/nembo kwenye shati lakini sisi hatukuwa na nembo..na
3...aah ngoja niishie hapo... turudi kwenye kwenye kisa.
Kipindi kile kilikuwa cha mbio za mweng,e basi mwenge ulikuwa unapita pale shuleni. Yule kiongozi wa mwenge kama tujuavyo anakuwa na ujumbe wa mwenge,basi akatoa ule ujumbe wa mwenge(hatasikumbuki ulikuwa nini?) Basi yule jamaa alipomaliza kwa sababu tulikuwa kimya mwanafunzi mmoja aliuwahi ule ukimya akamuuliza yule ndugu AAGH! yule kiongozi wa mwenge. (tena kwa sauti KUUBWAA) HADITHI HIYO KAKUFUNDISHA NANI?.... Basi nakwambia yule kiongozi wa mwenge alibaki mdomo wazi... na shule nzima ilipasuka kicheko. Kilichofuata mwenye unajua...(si adhabu)
Lengo langu la kukuambia kisa hiki ni kukumbusha kuwa kuna maswala mengi ambayo kwa njia moja ama nyingine ni vizuri mtu kuuliza hadithi hii kakufundisha nani?mfano.. Unaposoma kitabu, Gazeti, jarida, unaposikiliza hotuba za watawala,au majibu au utaratibu si vibaya kuuliza haditihi hhi kakufundisha nani au kamfundisha nani au Kuuliza alikwambia maana yake nini? Sio lazima uulize kwa sauti jaribu kujiuliza mwenye ili upate jibu litakalo kufaa. Kuna mambo mengi ambayo tumekuwa tukiyakubali bila kujua maana yake ni nini.
Nitaendelea Kukuletea mifano ya kujiuuliza ..... (ila usiniliuze sasa na wewe hadithi hii kanifundisha nani.teh..tehe..tehe) Baadae.

19 comments:

Simon Kitururu said...

Duh !Umeniacha hoi!Najaribu tu kufikiria jinsi kiongozi wa mwenge alivyopigwa mshangao.Ila naona wewe ulienda shule tofauti na mimi.Sisi ilikuwa kuchomekea na nembo ndio staili.

MTANZANIA. said...

Kuna falsafa imefichama hapa!
Mambo mengi ya kiofisi yanageuzwa kuwa kama hadithi kutoka kwa mababu. Sasa ni vema hadhira kutafuta maana halisi ya hadithi hizo.

Mija Shija Sayi said...

Umeniacha nacheka, hebu fikiria ungekuwa wewe ungejibu nini?

Ndabuli nadhani utakuwa umesomea kanda ya ziwa maana kule ndo kuna mambo ya lebo kwenye mashati, pia huko kuna vicheche wengi(jina mlilombatiza mwalimu).

mwandani said...

Falsafa kali hii. Kakufundisha nani?

Shule uliyoenda siwezi kuijua, mji niliosoma mimi kuchomekea ilikuwa wajibu, na kaptura lazima ifike magotini.

Ili kuvunja sheria wengine walikuwa wanakunja kaptura inakuwa kama bukta.

luihamu said...

Kaka Ndabuli,leo ni mara ya kwanza nabisha hodi katika nyumba yako.Nimekaribia mzee.Jah live.

NDABULI said...

@Da Mija,@mwandani ngoja niwape kidogo kidogo mpaka muweze kujua ni shule ipi. Hii shule haiko kanda ya ziwa, hii shule ni moja ya shule za zamani sana kanda ya mashariki ilikuwa zamani shule ya wahindi kabla ya uhuru. Miaka niliyosoma ilikuwa miaka ya 80, Lebo au kakitambaa kenye rangi kwenye shati vilitumika ila sisi hatukuwa nazo yaani kututofautisha na shule zingine sisi kutochomekea shati ndio ilikuwa alama yetu Ila sikuhizi nasikia wanachomekea na kuna lebo. Halafu ile mikondo(Kawaida si ina kuwa kama form 1 A,B,C, D..na kuendelea) kwetu ilikuwa ina annza na L,M,N,O haikuwepo ilirukia P,Q, na kuishia R.

NDABULI said...

Rasta Luihamu,Karibu,karibu sana, Jah bless!

Mija Shija Sayi said...

Hapa itabidi tukupe mji Ndabuli au?

NDABULI said...

Naona mnipe mji tu niwatajie

mwandani said...

nakupa mji wa mzizima

Anonymous said...

Nami nakupa huo huo wa Mzizima.

Mija Shija Sayi said...

Nenda Lindi.

mwandani said...

Vipi, unakataa mji?

NDABULI said...

Naona kweli mmepania kupata jibu, basi nakwenda Lindi,maana huko sijafika, Mzizima mmhh nimegoma (..aah sasa Ndesanjo na Mwandani msichukie sina hila yoyote na Da mija..heheh!). Jibu lake ni shule ya sekondari (napenda neno wakenya wanalotumia shule ya upili)AZANIA.Kama unamfahamu mtu aliye soma pale kati ya miaka ya 84-89 atakuwa anakumbuka hayo niliyosema. Ndesanjo, Mwandani, Mpo?

Mija Shija Sayi said...

Hivi Ndabuli unataka tupishane barabarani?

mwandani said...

Asante kwa jibu. kumbe nyie ndio mlikuwa majirani? miye nilikuwa mbele kidogo - tambaza - sijui vipi sikupata jibu!

NDABULI said...

@Mija sijakuelewa hiyo sentensi yako. @Mwandani kweli ilibidi ukumbuke maana nakumbuka enzi hizo tulikuwa watani wa Jadi kwenye michezo.

Mija Shija Sayi said...

Picha.

NDABULI said...

Da Mija, naogopa watu wataogopa kunitembelea/au watakuwa wanawatishia watoto picha maana hiyo sura yangu, hata yule jamaa aliyeshinda mashindano ya sura mbaya atajiona mzuri. Ila nikipita schiphol nitakustua tukipishana